Kupingwa kura ya kutokuwa na imani na Rais wa Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i29798-kupingwa_kura_ya_kutokuwa_na_imani_na_rais_wa_afrika_kusini
Katika hali ambayo, mjadala wa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini umegeuka na kuwa mkali kutoka upande wa wapinzani, Kamati ya Utendaji ya chama cha ANC imetaka kunyamaziwa na kufumbiwa macho suala hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2017 05:48 UTC
  • Kupingwa kura ya kutokuwa na imani na Rais wa Afrika Kusini

Katika hali ambayo, mjadala wa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini umegeuka na kuwa mkali kutoka upande wa wapinzani, Kamati ya Utendaji ya chama cha ANC imetaka kunyamaziwa na kufumbiwa macho suala hilo.

Baada ya kufanyika mkutano wa siku tatu wa Kamati ya Utendaji ya chama tawala cha ANC mjini Pretoria, mkuu wa kamati hiyo amezuia mpango wa kujadiliwa suala la kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Jacob Zuma. Kutokana na Rais Zuma kuwa na wafuasi wengi katika kamati hiyo, huko nyuma pia ameweza kuokoka na kashfa mbalimbali zilizomuandama kutokana na kupata himaya na uungaji mkono wa kamati hiyo.

Mgogoro wa kisiasa na malalamiko ya kijamii nchini Afrika Kusini yamechukua mkondo mpana zaidi katika miezi ya hivi karibuni. Licha ya kuwa, ni kwa muda sasa sakata la ufisadi limeshikiwa bango na wapinzani na kufuatiwa na malalamiko nchini humo, lakini hivi karibuni malamiko hayo yamechukua sura mpya baada ya Rais Zuma kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri. Katika mabadiliko hayo ya mwezi Machi mwaka huu, Rais Zuma aliwatia katika baraza hilo takribani shakhsia 10 ambao ni watu wake wa karibu. Hata hivyo hatua ya Rais Zuma ya kumfuta kazi Pravin Gordhan Waziri wa Fedha ilichochea zaidi moto wa upinzani dhidi yake na kuifanya serikali yake izidi kupelekwa mchakamchaka. 

Maandamano dhidi ya Rais Zuma

Rais wa Afrika Kusini alitaja sababu ya kumfuta kazi waziri huyo kwamba, ni katika juhudi za kupambana na ufisadi. Hata hivyo wapinzani wanapinga hilo na kusisitiza kwamba, Pravin Gordhan alifutwa kazi kwa sababu za kisiasa kutokana na waziri huyo kufichua upokeaji rushwa wa Rais Zuma. Weledi wengi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, marekebisho katika baraza la mawaziri, kilikuwa kisingizio cha Zuma kumfuta kazi  Pravin Gordhan.

Gordhan anayesifika kwa utendaji mzuri, alikuwa Waziri wa Fedha wa Afrika Kusini kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 na kisha baadaye Disemba mwaka jana akateuliwa tena kushika wadhifa huo. Tangu alipoteuliwa tena kushika wizara hiyo amekuwa akivutana na shaksia wa kisiasa wa chama tawala cha ANC. Mvutano huo ulianza baada ya waziri huyo kutoa matamshi akisisitiza kupambana na uongozi mbaya pamoja na udharura wa kufanyika mabadiliko katika muundo wa mashirika ya serikali. Pravin Gordhan mara kadhaa amesisitiza juu ya udharura wa kupambana na ufisadi nchini humo. Alikuwa na mpango wa kupunguza matumizi ya serikali, kuongeza kodi na kuifikisha nakisi ya bajeti ya nchi hadi asilimia 3.2 ya uzalishaji malighafi katika mwaka wa fedha wa 2016-2017. 

Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu

Tangu Rais Zuma alipoingia madarakani mwaka 2009 amekuwa akikabiliwa na mlolongo wa mafaili mbalimbali ya ufisadi wa kifedha ambapo miongoni mwazo ni hatua yake ya kutumia fedha za serikali kwa ajili ya kukarabati nyumba yake binafsi. Wapinzani wa Afrika Kusini wanasisitiza azma yao ya kutaka Rais Zuma aachie ngazi. Wapinzani hao wanafuatilia njia ya kisheria kama ya kupigwa kura ya siri  ya kutokuwa na imani na rais huyo. Hadi sasa Mahakama ya Katiba ya Johannesburg haijatoa idhini kwa wabunge kupiga kura ya siri ya kutokuwa na imani na Rais Zuma.

Hivi sasa hatua ya Kamati ya Utendaji ya chama cha ANC ya kutozungumzia suala la kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Rais Zuma kwa mara nyingine tena imeonyesha kuwa, chama hicho tawala kingali kinataka Zuma aendelee kubakia madarakani. Utendaji wa Rais Zuma licha ya kuwa umegubikwa na ukosoaji unaoongezeka wa ndani, lakini rais huyo ameahidi kuboresha hali ya uchumi. Disemba mwaka huu chama tawala cha ANC kinatarajiwa kukutana katika mkutano wake mkuu kwa ajili ya kumchagua mrithi wa Zuma ambaye atapeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2019.