UN: Ugonjwa wa kuharisha umeua watu 279 nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30414-un_ugonjwa_wa_kuharisha_umeua_watu_279_nchini_sudan
Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema kwa akali watu 279 wamepoteza maisha kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha nchini Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2017 08:58 UTC
  • UN: Ugonjwa wa kuharisha umeua watu 279 nchini Sudan

Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema kwa akali watu 279 wamepoteza maisha kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha nchini Sudan.

Taarifa iliyotolewa na OCHA hii leo ikinukuu ripoti ya Shirika la Afya Duniani WHO imesema, mbali na vifo hivyo 279, kesi 15 elfu za ugonjwa huo zimeripotiwa nchini Sudan tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi Juni 2 mwaka huu.

Imeongeza kuwa, asilimia 87 ya kesi hizo zimewaathiri watoto wadogo wenye chini ya umri wa miaka mitano, katika majimbo 11 ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Khartoum.

Wizara ya Afya ya Sudan imesema mbali na Khartoum, majimbo yaliyoathiriwa zaidi na mlipuko huo wa kuharisha ni White Nile, Senar na Kordofan Kaskazini huku ikitahadharisha kuwa yumkini hali ikawa mbaya zaidi kwa kuwa nchi hiyo inaelekea katika msimu wa mvua za masika.

Baadhi ya wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Sudan

Inaarifiwa kuwa, mlipuko huo wa ugonjwa wa kuharisha na kipindupindu katika baadhi ya maeneo nchini Sudan umesababishwa na ukosefu wa maji safi ya kunywa na vyoo, na umeripotiwa kushtadi kutokana na wimbi la wakimbizi wanaotoka nchi jirani ya Sudan Kusini. 

Zaidi ya raia 375,000 wa Sudan Kusini, asilimia 90 wakiwa ni wanawake na watoto, wamekimbia Sudan tokea vita vya ndani vianze katika nchi yao mwaka 2013.