UN inahitaji dola milioni 65 kwa ajili ya wakimbizi wa DRC
Umoja wa Mataifa umesema unahitaji makumi ya mamilioni ya dola kwa ajili ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliokimbilia nchi jirani ya Angola.
Taarifa ya Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR imesema taasisi hiyo na wafadhili wenza zinahitaji dola milioni 65 za Marekani kwa ajili ya wakimbizi raia wa Kongo wanaozidi kumiminika nchini Angola.
Zaidi ya wakimbizi 30,000 wameingia katika jimbo la Lunda Norte la Angola wakitokea Kongo DR tangu Aprili mwaka huu hadi sasa, idadi ambayo ni mara mbili ya ile iliyosajiliwa kabla ya Aprili.
UNHCR imesema inahitaji kwa dharura dola milioni 35 za Marekani kwa shabaha ya kuwapa bidhaa na huduma za msingi wakimbizi hao hadi mwishoni mwaka huu na kwamba kwa sasa mahitaji ya kibinadamu ya wakimbizi hao yanakidhiwa na dola milioni 10 zilizotolewa kutoka Mfuko wa Dharura wa Umoja wa Mataifa.
Raia hao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamekuwa wakikimbia mapigano yaliyozuka katika mkoa wa Kasai baina ya vikosi vya serikali na makundi ya wanamgambo katika eneo hilo.
Kuhusu wakimbizi wa ndani, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa, karibu wakimbizi 45 elfu wamekimbia makazi yao kutokana na kushadidi mapigano baina ya makundi yenye silaha katika jimbo la Kasai la katikati mwa nchi hiyo, na wameelekea upande wa kusini mwa nchi hiyo kubwa ya katikati mwa Afrika.