Jun 18, 2017 07:42 UTC
  • Watano wauawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu, Cairo, Misri

Mripuko mmoja wa bomu uliotokea kusini mwa Cairo, mji mkuu wa Misri umeua mtu mmoja na kujeruhi wengine wanne.

Televisheni ya Sky News imetangaza habari hiyo leo na kuongeza kuwa, mripuko wa bomu la kutengenezwa kienyeji lililokuwa limetegwa kando ya barabara umeua afisa mmoja wa polisi wa Misri na kuwajeruhi wengine wanne.

Hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mripuko huo, ingawa kidole cha lawama kinaelekezwa kwa kundi la Wilaya ya Sinai lenye mfungamano na genge la kigaidi la Daesh ambalo hadi sasa limeshafanya mamia ya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wanajeshi na polisi wa Misri.

Mwanajeshi wa Misri akiimarisha ulinzi mbele ya kanisa moja nchini humo

 

Itakumbukwa kuwa jana Jumamosi mahakama moja nchini Misri iliwahukumu adhabu ya kifo watu 31 kwa tuhuma za kushiriki katika mauaji ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa zamani wa nchi hiyo.

Habari hizo zimesema kuwa, mahakama ya jinai ya kusini mwa Cairo, jana Jumamosi imewahukumu adhabu ya kifo watuhumiwa 31 wanaohusishwa na mauaji ya Hisham Muhammad Zaki Barakat, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa zamani wa nchi hiyo na faili la kesi yao limepelekwa kwa Mufti wa Misri ili lipate idhini ya kisheria.

Mahakama hiyo imesema kuwa, watuhumiwa hao 31 ni wanachama wa kundi moja haramu na wamehusika katika mauaji ya makusudi yaliyopangwa kabla na pia kwa kosa la kumiliki silaha za moto kinyume cha sheria.

Hisham Barakat, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa zamani wa Misri aliuawa kwa bomu lililokuwa limetegwa kwenye gari yake tarehe 29 Juni, 2015, mjini Cairo. Kundi linalojiita la mapambano ya wananchi lilitangaza kuhusika na shambulio hilo. 

Tags