Mahakama Afrika Kusini yapiga marufuku shule kutangaza dini yoyote
Mahakama moja nchini Afrika Kusini leo Jumatano imeamuru kuwa, taasisi za elimu za umma hazipaswi kueneza na kutangaza dini moja pekee na kuziweka kando dini nyingine, ikisema kuwa kufanya hivyo ni kukiuka Hati ya Shule.
Amri hiyo ya marufuku imetolewa na Jaji Willen Van der Linde. Taasisi ya Elimu ya Kidini na Demokrasia ya nchini Afrika Kusini (OGOD) imesema kwamba ilikuwa ni kwa maslahi ya demokrasia ya nchi hiyo shule za umma kutoruhusiwa kupendelea dini fulani.
Taasisi hiyo ya OGOD imeitaka mahakama hiyo ya Afrika kusini kutangaza sera za kidini zinazoendeshwa na shule sita za umma nchini humo kuwa ni kinyume na katiba; na kuzituhumu shule hizo kuwa zinaipendelea dini ya Kikristo mkabala ya dini nyingine.
Naye Waziri wa Elimu wa Afrika kusini Angie Motshekga ameunga mkono agizo hilo na kusema kuwa ni marufuku kwa shule za Afrika Kusini kupendelea dini moja dhidi ya dini nyingine.