Wanamgambo sita wa al-Shabab wauawa na jeshi la Somalia
Vikosi vya usalama vya Somalia vimewaua wapiganaji sita wa kundi la kigaid na kitakfiri la al-Shabab na kujeruhiwa makumi ya wengine.
Abdullah Ali mmoja wa makamanda wa jeshi la taifa la Somalia amesema kuwa, wapiganaji hao wa al-Shabab wameuawa na jeshi la nchi hiyo baada ya kushambulia kituo kimoja cha jeshi katika mji wa Shebelle ya Kati kusini mwa nchi hiyo.
Kamanda huyo wa jeshi la Somalia amesema kuwa, katika mapigano hayo wanamgambio sita wa kundi la kigaidi la al-Shabab wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Aidha amesema kuwa, mwanajeshi mmoja wa Somalia amepoteza maisha yake katika mapigano hayo.
Wanamgambo wa al-Shabab wameshadidisha mashambulio yao katika siku za hivi karibuni dhidi ya vituo vya serikali na vya kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika AMISOM.
Ingawa kundi la magaidi wa al-Shabab limefurushwa katika miji yote mikubwa na maeneo muhimu ya Somalia, lakini bado wanamgambo wake katika baadhi ya vijiji na miji hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na maafisa wa serikali.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Umoja wa Afrika ulitangaza kuwa, umeazimia kurejesha amani na utulivu nchini Somalia licha ya kuongezeka mashambulio ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.