Wanane wauawa na kujeruhiwa karibu na Mogadishu Somalia
Watu wanane wameripoti kuuawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea karibu na Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, jeshi la polisi la Somalia limetangaza kuwa, watu wawili wameuawa ambao walikuwa ni mwanamke mmoja na dereva mwanamme wakati basi dogo walilokuwa wakisafiria kukanyaga bomu la kutegwa barabarani mashariki mwa Mogadishu. Abiria wengine sita wamejeruhiwa katika shambulizi hilo. Wote waliouawa na kujeruhiwa walikuwa ni raia wa kawaida.
Hadi tunapokea habari hii hakukuwa na kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo. Hata hivyo kidole cha lawama kinaelekewa kwa genge la kigaidi la al Shabab ambalo ndilo lenye historia ya kufanya mashambulio kama hayo nchini Somalia.
Kundi la al Shabab linadai kuwa lengo lake ni kuipindua serikali ya Somalia. Hata hivyo mashambulizi ya genge hilo ndani na nje ya Somalia yanawalenga zaidi raia wa kawaida.
Ijapokuwa wamefurushwa katika miji yote mikuu ya Somalia, lakini hadi hivi sasa magaidi wa al Shabab wanadhibiti baadhi ya vijiji vya nchi hiyo na mara kwa mara wanafanya mashambulizi na jinai dhidi ya maeneo ya umma na ya raia na wakati mwingine katika maeneo ya kijeshi ili kujaribu kuonesha kuwa bado wapo.