Mar 15, 2016 15:24 UTC
  • Iran yalaani hujuma ya kigaidi nchini Ivory Coast

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani hujuma ya kigaidi ya hivi karibuni iliyosababisha watu 19 kuuawa nchini Ivory Coast.

Hussein Jaberi Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo na kusema kuwa taifa la Iran linasimama nao pamoja na serikali ya Kodivaa wakati huu wanapoomboleza. Ansari amesisitiza haja ya kuungana jamii ya kimataifa ili kutokomeza harakati za kigaidi duniani. Hii ni katika hali ambayo, Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast ametoa wito kwa nchi za eneo la magharibi mwa Afrika kuunda muungano wa kupambana na kulishinda janga la ugaidi. Rais wa Ivory Coast ametoa wito huo kufuatia shambulio la kigaidi la siku ya Jumapili dhidi ya hoteli za ufukweni katika eneo la Grand Bassam na kusisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuwa pamoja na nchi nyingine katika Jamii ya Kimataifa ili kuhakikisha ugaidi unatokomezwa. Wakati huohuo ripoti kutoka Ivory Coast zinaeleza kuwa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na shambulio la siku ya Jumapili imeongezeka na kufikia 19. Kundi la kigaidi la Al-Qaeda katika eneo la kaskazini mwa Afrika (AQIM) limetangaza kuwa ndilo lililohusika na shambulio hilo.

Tags