Wapalestina wapongeza hatua ya Afrika Kusini kupunguza uhusiano na Israel
Wapalestina wamepongeza uamuzi wa hivi karibuni wa chama tawala cha Afrika Kusini ANC, ya kupunguza kiwango cha uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika kikao cha sera za chama cha Africa National Congress ANC, huko Johannesburg siku chache zilizopita, kamati ya uhusiano wa kimataifa ya chama hicho ilitangaza uamuzi wa kupunguza hadhi ya ubalozi wa Afrika Kusini huko Tel Aviv na kuufanya uwe ofisi ya mawasiliano tu. Hatua hiyo imechukuliwa na ANC kama njia ya kuonyesha "msimamo usioterereka wa kuunga mkono mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina na kulaani hatua zinazochukuliwa na utawala wa Israel za kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kukiuka sheria za kimataifa."

Mkuu wa kamati ya uhusiano ya kimataifa ya ANC Mirima Segabutla amesema uamuzi wa kupunguza hadhi ya ubalozi wa Afrika Kusini huko Israel ni ujumbe wenye nguvu kwa ajili ya kupinga hatua za Israel kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kukiuka haki za Wapalestina.
Katika taarifa Jumamosi, msemaji wa Hamas Hazem Qasim amepingeza ANC kwa uamuzi huo na kutoa wito wa kushinikizwa zaidi Israel ili itambue haki za Wapalestina. Naye Hashem Dajani, balozi wa Palestina nchini Afrika Kusini ameutaja uamuzi wa ANC kuwa hatua moja mbele katika kuushinikiza utawala wa ubaguzi wa rangi wa Israel ili usitishe ukaliaji mabavu nchi ya Palestina.