Watu 8 wauawa na 50 kujeruhiwa katika shambulio la guruneti Burundi
Watu wanane wameuawa na wengine hamsini wamejeruhiwa katika kijiji kimoja mkoani Kayanza kaskazini mwa Burundi juzi jioni. Pierre Nkurikiye Msemaji wa Polisi ya Burundi amesema kuwa watu wanne waliaga dunia papo hapo katika eneo la tukio na wengine wanne walifariki kwa majeraha waliyopata katika shambulio hilo la guruneti.
Msemaji wa polisi ya Burundi ameongeza kuwa shambulio hilo la guruneti lilitekelezwa jioni ya juzi Jumapili majira ya sasa 12 na nusu kwa wakati wa Burundi katika kijiji cha Shinya. Nkurikiye ameitaja hujuma hiyo kuwa ni shambulizi la kigaidi.
Msemaji wa polisi ya Burundi amesema kuwa mtu asiyefahamika alirusha guruneti katika umati wa watu. Itakumbukwa kuwa watu wasiopungua 700 waliuawa katika ghasia za kisiasa kati ya wafuasi wa Rais Nkurunziza na wa upinzani tangu mwezi Aprili mwaka 2015, wakati Rais huyo wa Burundi alipotangaza nia yake ya kugombea kiti cha rais kwa mara ya tatu.