Mlipuko wa guruneti waikumba Bujumbura, watu kadhaa wajeruhiwa
Watu kadhaa wamejeruhiwa katika mlipuko uliotokea Bujumbura mji mkuu wa Burundi.
Karibu watu kumi wamejeruhiwa kufuatia mlipuko wa guruneti uliotokea jana usiku mbele ya mgahawa mmoja katika eneo la Bwiza katika mji mkuu Bujumbura. Ripoti zinasema kuwa kuna uwezekano mkubwa idadi ya majeruhi ikaongezeka. Duru za kuaminika nchini Burundi zimeeleza kuwa watu waliohusika na mipuko huo wa guruneti wamekimbia. Mashambulizi ya guruneti yameongezeka pakubwa huko Burundi katika siku za hivi karibuni.
Burundi imekumbwa na ukosefu wa amani na ghasia za kisiasa tangu mwezi Aprili mwaka juzi baada ya wananchi na vyama vya kisiasa kupinga kuongezwa muhula wa kusalia madrakani Rais Pierre Nkurunziza kwa muhula wa tatu kinyume na katiba ya nchi hiyo. Tangu wakati huo hadi sasa, raia wa Burundi zaidi ya 500 wameuawa katika mchafuko na mapigano ya mitaani huku wengine zaidi ya laki tatu wakiyahama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.