Mamilioni ya fedha za umma za mauzo ya madini zatoweka Congo DR
Jumuiya ya kimataifa ya Global Witness imetangaza kuwa, asilimia 20 ya mapatano yanayotokana na mauzo ya madini ya almasi, dhahabu na shaba zimetoweka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti iliyotolewa na Global Witness imesema kuwa, dola zisizopungua milioni 750 za mapato ya umma ya madini zimetoweka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kwamba fedha hizo zimegawanywa kwa njia za kifisafi katika mitandao yenye mfungamano na Rais Joseph Kabila.
Global Witness imesisitiza kuwa, mapato ya madini ya almasi, dhahabu na shaba yamekuwa yakitumbukizwa katika akaunti za kampuni ya madini ya Gecamines na mengine yanawekwa katika akaunti za benki za watu binafsi na mitandao ya kiuchumi yenye mfungamano na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hata hivyo serikali ya Kinshasa imekanusha habari ya kutoweka mapato ya madini ya almasi, dhahabu na shaba na kudai kuwa, fedha zilizotumwa katika akaunti za benki za watu binafsi na mitandao ya kiuchumi kwa hakika zinahusiana na matumizi ya serikali.

Kutoweka kwa mapato ya taifa ya madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumekuwa na taathira ya moja kwa moja katika kushuka chini thamani ya sarafu ya nchi hiyo na kupanda gharama za maisha.
Jumuiya ya kimataifa ya Global Witness inasema, mapato yanayotokana na mauzo ya madini kama almasi na dhahabu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanapaswa kutumika katika kugharamia masuala ya umma kama shule, mahospitali na kadhalika.