ANC yapinga safari ya ujumbe wa Israel Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i32842-anc_yapinga_safari_ya_ujumbe_wa_israel_afrika_kusini
Msemaji wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amesema kuwa, chama hicho hakitakutana na ujumbe wa Israel utakaotembelea nchi hiyo mwezi huu wa Agosti kutokana na uhalifu na jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 07, 2017 22:34 UTC
  • ANC yapinga safari ya ujumbe wa Israel Afrika Kusini

Msemaji wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC amesema kuwa, chama hicho hakitakutana na ujumbe wa Israel utakaotembelea nchi hiyo mwezi huu wa Agosti kutokana na uhalifu na jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.

Nonceba Mhlauli amesema kuwa, iwapo ujumbe wa Israel utatembelea Afrika Kusini basi wabunge wa nchi hiyo hawatashiriki katika vikao au shughuli yoyote ya ujumbe huo. 

Amesisitzia kuwa, wabunge wa ANC hawataki kuona ujumbe wa Israel ukiingia katika Bunge la nchi hiyo na iwapo utaruhusiwa kuingia basi wabunge hao hawatahudhuria kikao hicho. 

Wakati huo huo Mandla Mandela, mjukuu wa shufaa wa uhuru wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela ameunga mkono uamuzi wa wabunge wa chama tawala cha ANC na kutangaza kuwa, msimamo huo unaonesha jinsi Bunge la Afrika Kusini linavyofungamana na suala la kuwatetea watu wa Palestina.

Mandla Mandela

Mandla ametoa wito wa kufukuza balozi wa Israel nchini Afrika Kusini, kurejeshwa nyumbani balozi wa nchi hiyo kutoka Tel Aviv na kukatwa uhusiano na utawala huo wa Kizayuni. Mjukuu wa Mzee Nelson Mandela amesema, nchi zote duniani zinapaswa kutekeleza majukumu yao ya kibinadamu ya kukabiliana na utawala katili na haramu wa Israel.