UN: Tunafuatilia kwa karibu uchaguzi wa Kenya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo unafuatilia kwa karibu zoezi la uchaguzi mkuu linalofanyika hii leo nchini Kenya.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN amesema kupitia msemaji wake kuwa, chombo hicho cha kimataifa kinataraji kuwa uchaguzi huu utakuwa wa huru na haki na utafanyika katika mazingira ya amani na uwazi.
Kadhalika amesisitizia umuhimu wa vyombo vya usalama kuheshimu haki za binadamu katika kipindi hiki ambapo Wakenya wanatekeleza haki yao ya kidemokrasia.
Hii ni katika hali ambayo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiserikali wa Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) imewatolea wito washika dau wote katika uchaguzi mkuu wa Kenya kuhakikisha kuwa uchaguzi wa leo unafanyika kwa amani na utulivu.
Awali, Thabo Mbeki, Rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye anaongoza timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika AU nchini Kenya alisema wananchi wa taifa hilo la Afrika Mashariki wanataka kuona zoezi hilo linafanyika katika mazingira huru, yenye haki na uwazi.
Huku hayo yakirifiwa, Wakenya wameripotiwa kurauka alfajiri na mapema na kuelekea katika masanduku ya kupiga kura kuchagua viongozi wao, akiwemo rais, wabunge, magavana na wawakilishi wa wadi. Katika uchaguzi wa rais, mchuano mkali unatarajiwa kati ya Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee anayewania muhula wa pili, na kinara wa muungano wa upinzani wa NASA Raila Odinga, anayegombea kiti hicho kwa mara ya nne sasa.