Igad: Uchaguzi mkuu Kenya umefanyika kwa amani, uwazi na utaratibu sahihi
Timu ya wasimamizi wa uchaguzi ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiserikali wa Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika (Igad) imeipongeza Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) kwa kusimamia uchaguzi kwa njia sahihi na kusema kuwa, tume hiyo inapaswa kuwa kigezo cha kuigwa na nchi nyingine za Afrika.
Akizungumza leo mjini Nairobi, balozi Tewolde Gebremeskel anayeongoza timu ya wasimamizi wa Igad katika uchaguzi wa Kenya amesema: Tathmini ya awali inaonesha kuwa, uchaguzi mkuu umefanyika kwa amani, uwazi na utaratibu sahihi.
Balozi Gebremeskel ameongeza kuwa, zoezi la uchaguzi mkuu wa Kenya limefanyika kwa mujibu wa Katiba na utawala wa sheria.
Mkurugenzi wa Idara ya Amani na Usalama ya Igad amewataka wanasiasa na vyama vya siasa kuheshimu matakwa ya wananchi.
Balozi Tewolde Gebremeskel amesema, Igad itatoa ripoti kamili kuhusu uchaguzi mkuu wa Kenya katika wakati mwafaka lakini amesisitiza kuwa, zoezi hilo liefanyika kwa njia ya kuridhisha.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha NASA Bwana Raila Odinga amepinga matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu nchini Kenya akisema yamechakachuliwa.