Aug 10, 2017 03:03 UTC
  • Wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu wauawa CAR

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limeripoti kuwa, wafanyakazi wake kadhaa wameuawa katika shambulizi lililofanywa na waasi huko kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu imesema kuwa: Wafanyakazi sita wa kujitolea wa shirika hilo wameuawa katika shambulizi lililofanywa na waasi wanaobeba silaha dhidi ya kituo kimoja cha afya kusini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kuna uwezekano kwamba wahudumu wa afya na raia wa kawaida pia wameuawa katika shambulizi hilo. 

Semina ya wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu, CAR

Wafanyakazi hao sita waliouawa wa shirika la Msalaba Mwekundu walikuwa wakishiriki mkutano wa hali ya mgogoro katika kituo cha afya cha mji wa Gambo katika mkoa wa Mbomou.

Hilo ni shambulizi la tatu kufanywa dhidi ya wafanyakazi wa Shirika la Msalaba Mwekundu kwa mwaka huu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati likiwemo lile la mwezi Juni katika mji wenye mgodi wa dhahabu wa Bangassou.   

Tags