Watu 5 wameuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu Kenya
Watu 5 wameripotiwa kuuawa katika ghasia na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika juzi nchini Kenya baada ya kinara wa kambi ya upinzani, Raila Odinga kudai kuwa kumefanyika udanganyifu mkubwa.
Mkuu wa polisi ya Nairobi Japheth Koome amesema kuwa, watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi jana akisisitiza kuwa walitumia machafuko kupora mali za watu.
Mtu mwingine mmoja aliuawa mapema jana kwa kupigwa risasi na polisi katika kaunti ya Kisii nje ya Shule ya Sekondari ya Nduru ambayo ilikuwa na kituo cha kuhesabu kura za uchaguzi wa rais katika jimbo la uchaguzi la Mugirango.
Huko kusini mashariki mwa mkoa wa Tana River polisi imesema kuwa, watu watano waliokuwa na silaha baridi walivamia kituo cha kupigia kura na kumuua kwa kumdunga kisu raia mmoja. Mkuu wa polisi ya eneo hilo, Larry Kieng amesema kuwa askari usalama waliwafyatulia risasi watu wa kundi hilo na kuua wawili miongoni mwao.
Kieng amesema polisi inawasaka waliokimbia na kwamba hadi sasa haijajulikana iwapo hujuma hiyo ilifanyika kwa sababu za kisiasa au ni jinai na uhalifu wa kawaida.
Katika mji wa Kisumu ambao ndiyo ngome kuu ya kinara wa upinzani Raila Odinga, polisi ilitumia gesi ya kutoa machozi na risasi kutawala waandamanaji waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa rais.
Matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC) yanaonesha kuwa, mgombea wa chama cha Jubilee, Uhuru Kenyatta anaongoza kwa kura milioni saba na laki 9 na 63 elfu ambazo ni sawa na asilimia 53.89 ya kura zilizohesabiwa huku mpinzani wake mkuu, Raila Odinga akiwa na kura milioni sita na laki tano na sabini elfu ambazo ni sawa na asilimia 44.47 ya kura.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha NASA Bwana Raila Odinga amepinga matokeo hayo akisema yamechakachuliwa.