Polisi yashutumiwa kwa kuvamia ofisi za asasi zisizo za serikali Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33228-polisi_yashutumiwa_kwa_kuvamia_ofisi_za_asasi_zisizo_za_serikali_kenya
Mashirika ya kiraia na yale ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali hatua ya vyombo vya dola ya kuvamia na kutaka kufunga kwa nguvu ofisi ya asasi isizo ya serikali katika mji mkuu Nairobi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 16, 2017 14:27 UTC
  • Polisi yashutumiwa kwa kuvamia ofisi za asasi zisizo za serikali Kenya

Mashirika ya kiraia na yale ya kutetea haki za binadamu yamekosoa vikali hatua ya vyombo vya dola ya kuvamia na kutaka kufunga kwa nguvu ofisi ya asasi isizo ya serikali katika mji mkuu Nairobi.

Hii ni baada ya maafisa wa polisi na wale wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kuvamia ofisi ya asasi ya kiraia inayopigania demokrasia na uwazi barani Afrika (AfriCOG) jijini Nairobi hii leo, siku moja baada ya Bodi ya Kusimamia Asasi Zisizo za Serikali kumwandikia barua Mkuu wa Idara ya Makosa ya Jinai na KRA kudai kuwa AfriCOG halijasajiliwa na limekuwa likikwepa kulipa kodi.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Afrika lenye makao yake makuu mjini Mombasa limekosoa uvamizi huo na kusema mkondo huo utaipeleka pabaya nchi.

Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo Fred Matiang'i ameingilia kati na kuiagiza Bodi ya Kusimami Asasi Zisizo za Serikali kutochukua hatua yoyote dhidi ya asasi hiyo na ile ya Kamisheni ya Haki za Binadamu KHRC, katika kipindi cha siku 90 zijazo.

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo Fred Matiang'i

Katika hatua nyingine, Umoja wa Ulaya umeitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC) ichapishe matokeo yote katika tovuti yake ili kuwahakikishia wananchi kwamba iliendesha zoezi hilo kwa uwazi na usahihi. Hii ni baada ya msemaji wa IEBC, Andrew Limo kusema kuwa hadi sasa hawajatuma kwenye tovuti ya tume hiyo, fomu 2,900 kati ya 41,000 za kuonyesha matokeo ya vituo vya kupiga kura. 

IEBC ilimtangaza Rais Uhuru Kenyatta aliyegombea kwa chama cha Jubilee mshindi wa kura za rais na kumbwaga mpinzani wake wa karibu Raila Odinga, aliyewania kupitia ODM, chama tanzu katika muungano wa NASA.