Aug 21, 2017 08:22 UTC
  • Mapigano yashadidi katika mji wa Bria Jamhuri ya Afrika ya Kati

Mapigano makali yameripotiwa kati ya makundi ya Seleka na Anti-Balaka katika mji wa Bria wa katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuua zaidi ya watu 10.

Duru za afya mjini Bria zimetangaza kuwa, katika mapigano hayo yaliyoanza siku ya Jumamosi iliyopita watu 13 wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa. Habari zaidi zinasema kuwa, akthari ya watu waliojeruhiwa katika mapigano hayo ni wanachama wa makundi mawili. Duru za afya zimeongeza kuwa, mapigano yaliyojiri kati ya makundi ya Seleka na Anti-Balaka kuanzia siku za Jumanne na Jumatano wiki iliyopita yamesababisha karibu watu 30 kuuawa.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Kikristo Anti-Balaka

Wasimamizi wa amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mjini Bria wametangaza utayarifu wao kwa ajili ya kuzuia kuibuka mapigano mapya kati ya makundi hayo mjini Bria.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013 baada ya kundolewa madarakani rais wa zamani wa taifa hilo François Bozizé. Tangu alipoingia madarakani Rais Faustin-Archange Touadéra nchini humo bado hajaweza kuzuia mapigano na kurejesha usalama.

Tags