Kundi la al-Shabaab la Somalia ladai kuua makumi ya askari Kismayu
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limedai kuwa limeua makumi ya askari wa Somalia karibu na mji wa bandari wa Kismayu mapema leo Jumapili.
Msemaji wa genge hilo Abdiasis Abu Mus'ab amesema wanachama wa kundi hilo la ukufurishaji wameshambulia kituo cha kijeshi katika eneo la Jubaland, karibu na mji wa Bula Gudud na kuua wanajeshi 26.
Ameongeza kuwa, askari wengine kadhaa wamejeruhiwa na kwamba kundi hilo la kigaidi limeteketeza moto magari mawili na kuondoka na mawili kutoka kituo hicho cha jeshi.
Wakazi wa eneo hilo wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, maafisa wa jeshi la Somalia wamethibitisha kutokea uvamizi huo.
Shambulio hili linajiri siku mbili baada ya watu 12 kuuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na genge hilo la kigaidi na kitakfiri katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia Ijumaa iliyopita, wakati wa sherehe za Idd-ul-Adh'ha.
Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianzisha mashambulizi yake nchini Somalia mwaka 2006.