Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusiana na kuongezeka machafuko nchini Burundi
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusiana na kuongezeka utumiaji mabavu na vitendo vya utesaji katika nchi ya Burundi.
Zeid Raad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameashiria katika kikao maalumu cha Baraza la Usalama la umoja huo kuhusiana na Burundi juu ya kuendelea vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na kupewa kinga wanaofanya vitendo hivyo na kubainisha kwamba, hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, maafisa wa haki za binadamu wa umoja huo hivi karibuni walitembelea vituo wanakoshikiliwa watu katika mji mkuu, Bujumbura na kushuhudia jinsi watu hao walivyoteswa na kufanyiwa muamala mbaya.
Machafuko ya ndani nchini Burundi yalianza baada ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kutangaza nia yake ya kuwania tena kiti hicho kwa mara ya tatu mfululizo. Wapinzani wanasema hatua hiyo ilikiuka katiba ya nchi na makubaliano ya amani ya Arusha, Tanzania yaliyohitimisha vita vya ndani katika nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, tangu Aprili mwaka 2015 hadi sasa wakimbizi laki tano na 946 wa Burundi wamekimbilia katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Tanzania, Rwanda, Uganda na Zambia.