Burundi yakanusha ripoti ya UN inayoituhumu kukiuka haki za binadamu
Serikali ya Burundi imekanusha vikali ripoti iliyotolewa Jumatatu iliyopita na Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, inayoielekezea kidole cha lawama maafisa usalama kwa mauaji, jinai na ukiukaji wa haki za binadamu unaoshuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2015.
Katika mapendekezo yake, wataalamu wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuanzisha uchunguzi mara moja na kuwapandisha kizimbani wahusika kabla ya Oktoba 16, tarehe ambayo mchakato wa nchi hiyo ya Kiafrika kujiondoa kwenye Mkataba wa Roma ulionda ICC utakuwa umekamilika.
Ripoti za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, watu kati ya 500 hadi 2000 wameuawa katika machafuko ya Burundi, mamia wametoweka na wengine wengi kuteswa vikali.
Willy Nyamwite, msemaji wa serikali ya Burundi amesema ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inaegemea upande mmoja na kwamba madai yaliyomo kwenye ripoti hiyo hayana msingi wowote.
Naye Waziri wa Masuala ya Haki za Binadamu nchini humo Martin Nivyabandi ameitaka Kamisheni hiyo ya Umoja wa Mataifa kuwasilisha orodha hiyo kwa serikali ili wahusika waadhibiwe kwa mujibu wa sheria nchini Burundi.
Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.
Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba, ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania.