Wakimbizi 300 waanza kurejea Burundi kutoka Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34019-wakimbizi_300_waanza_kurejea_burundi_kutoka_tanzania
Awamu ya kwanza ya wakimbizi wa Burundi wanaorejea kwa hiari kutoka Tanzania wanatarajiwa kuwasili nchini mwao leo.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Sep 07, 2017 07:46 UTC
  • Wakimbizi 300 waanza kurejea Burundi kutoka Tanzania

Awamu ya kwanza ya wakimbizi wa Burundi wanaorejea kwa hiari kutoka Tanzania wanatarajiwa kuwasili nchini mwao leo.

Awamu ya kwanza ya wakimbizi wa Burundi wanaorejea kwa hiari kutoka Tanzania wanatarajiwa kuwasili nchini mwao leo.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mapatano ya juma lililopita kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, serikali ya Tanzania na Burundi.

Abel Mbilinyi, Mwakilishi Mkazi wa UNHCR nchini Burundi amethibitisha kurejea  kwa awamu ya kwanza ya wakimbizi wa Burundi, itakayoshuhudia kurejea takribani wakimbizi 300 ambao watafika vituo vinne vilivyo katika maeneo ya mashariki na kusini mwa Burundi pamoja na mji mkuu Bujumbura.

Kadhalika amezungumzia changamoto katika mchakato huo wa kuwarejesha kwa hiari wakimbizi hao wa Burundi wanaorejea kutoka Tanzania na kusema kuna upungu wa fedha za kuwahudumia wakimbizi hao. Ametoa wito kwa wafadhili kuwasaidia wakimbizi hao. Amesema UNHCR inasisitiza kuwa wakimbizi wanapaswa kurejea nyumbani kwa hiari na wasikumbwe na hatari wanaporejea. Inatabiriwa kuwa hadi kufika mwisho wa mwaka huu, wakimbizi 12,000 wa Burundi walio Tanzania watarejea makwao. Kuna wakimbizi takribani 250,000 wa Burundi katika kambi mbali mbali nchini Tanzania.

Rais Nkurunziza wa Burundi

Hayo yanajiri wakati ambao wiki hii Serikali ya Burundi imekanusha vikali ripoti iliyotolewa Jumatatu iliyopita na Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, inayowaelekezea kidole cha lawama maafisa usalama kwa mauaji, jinai na ukiukaji wa haki za binadamu unaoshuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2015.

Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.

Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba, ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania. Hata hivyo serikali ya Burundi inasisitiza kuwa haijakiuka mapatano ya Arusha.