Tanzania: Tuna mahindi ya ziada, tutaanza kuuza Kongo DR na Sudan Kusini
Serikali ya Tanzania imesema mazungumzo yanaendelea ili nchi hiyo ya Afrika Mashariki ianze kuuza mahindi kwenye Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Sudan Kusini.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Tanzania, William ole Nasha alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) aliyetaka kujua ni kwa nini serikali inazuia wakulima kuuza mazao yao nje ya nchi.
Ole Nasha amenukuliwa na gazeti la serikali la Habari Leo akisema kuwa, lengo la serikali kuzuia kuuza mazao nje ya nchi, ni kuhakikisha taifa linakuwa na usalama wa chakula nchi nzima.
Haya yanajiri siku mbili baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), Jose Graziano da Silva kumhakikishia Rais John Magufuli wa Tanzania kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Tanzania kufanya mageuzi katika kilimo kwa kuwezesha uzalishaji wa mazao na viwanda vya mazao hayo.
Graziano da Silva alisema hayo katika Ikulu ya Dar es Salaam muda mfupi baada ya kufanya mazungumzo na Rais Magufuli na kumshukuru kwa ushirikiano mzuri ambao shirika hilo limeupata kwa kipindi cha miaka 40 ya uwepo wake nchini humo.