Ki-moon: Viongozi wa kisiasa Burundi waonyeshe ushujaa wao kupitia mazungumzo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon ameitaka serikali na viongozi wa upinzani nchini Burundi, kufanya mazungumzo yenye itibari ili kumaliza mgogoro wa nchi hiyo.
Ban amesema kuwa, serikali na wapinzani wanatakiwa kuonyesha ushujaa wao kwa kuanzisha mazungumzo hayo kwa maslahi. Ameongeza kuwa, hakuna njia nyingine ghairi ya udiplomasia wa kisiasa inayofaa kutatua migogoro iliyoenea katika nchi zote za dunia hii leo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonyesha wasi wasi wake juu ya hali mbaya ya mambo nchini Burundi, licha ya viongozi wa serikali kumhakikishia kurejea usalama kwa hatua, wakati alipoitembelea nchi hiyo hivi karibuni. Kwa mujibu wa takwimu za mwisho za Umoja wa Mataifa, watu 400 wameuawa hadi sasa katika machafuko yaliyoibuka tangu mwezi April mwaka jana na zaidi ya laki mbili na nusu wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo. Kung'ang'ania madaraka Rais Pierre Nkurunziza, kunatajwa kuwa chanzo kikuu cha mgogoro huo unaozidi kupanuka siku hadi siku nchini humo. Hii ni katika hali ambayo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusiana na kuongezeka utumiaji mabavu na vitendo vya utesaji nchi ya Burundi.