Serikali ya Kongo DR yaanza uchunguzi kuhusu mauaji ya wakimbizi wa Burundi
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema kuwa imeanza kuchunguza mauaji ya makumi ya wakimbizi wa Burundi waliouliwa nchini humo.
Lambert Mende msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza kuwa baadhi ya watu waliouawa ni wanachama wa kundi moja linalobeba silaha na kwamba serikali tayari imeanzisha uchunguzi wa kisheria kuhusu mauaji ya makumi ya wakimbizi hao wa Burundi. Msemaji wa serikali ya Kongo ameongeza kuwa wanafanya uchunguzi huo si kufuatia ombi la Umoja wa Mataifa bali ni serikali ya Kinshasa yenyewe ndiyo iliyoamua kufanya hivyo.
Wakimbizi wa Burundi walipigwa risasi na wanajeshi wa Kongo Ijumaa usiku iliyopita wakati walipokuwa wakiandamana katika mji wa Kamanyola mkoani Kivu ya Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kusababisha vifo vya waandamanaji 36 ambao walikuwa ni wakimbizi kutoka Burundi.
Imebainika kuwa wakimbizi hao wa Burundi walikuwa wakidai kuachiwa huru wenzao ambao walitiwa nguvuni Jumatano iliyopita na kuamuriwa kuondoka huko Kongo. Serikali ya Burundi kwa upande wake imetaka kufanyika uchunguzi na kuwaomba viongozi wa Kinshasa wawasilishe maelezo kuhusu mauaji hayo. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, wakimbizi wa Burundi elfu 44 wamepewa hifadhi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.