Waziri wa Afrika Kusini akitaka chama ANC kimuadhibu Zuma
Waziri wa Nyumba na Makazi wa Afrika Kusini, Lindiwe Sisulu leo amesema kuwa chama tawala nchini humo ANC kinapasa kumuadhibu Rais Jacob Zuma kwa kukisababishia chama hicho sifa mbaya.
Matamshi hayo ya Sisulu yanahesabiwa kuwa mashambulizi mapya zaidi kufanywa na waitifaki wa zamani wa Zuma dhidi ya kiongozi huyo huku chama hicho tawala kikiendelea kuyumba kabla ya kufanyika mkutano wake mwezi Disemba mwaka huu wa kumchagua kiongozi mpya wa chama. Rais Zuma anaweza kuendelea kuwa Rais wa nchi hadi wakati wa kufanyika uchaguzi wa Bunge mwaka 2019.
Bi Sisulu ni waziri wa siku nyingi ambaye anatoka katika familia mashuhuri kwa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi (Apartheid) na anatambulika kama shakhsia mtarajiwa anayeweza kumrithi Jacob Zuma. Bi Lindiwe Sisulu ameeleza kuwa ripoti iliyowalishwa mwezi Julai katika mkutano wa sera wa ANC iligundua kuwa, kashfa zinazomkabili Zuma zimesababisha hali ya mivutano na wasiwasi ndani ya chama hicho.
Wanachama wa chama tawala ANC cha nchini Afrika Kusini katika miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakimtaka Zuma ajiuzulu kufuatia silsila ya kashfa zinazomkabili.