UN yajitosa katika uchaguzi wa marudio Kenya, wapinzani kuandamana dhidi ya IEBC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34865-un_yajitosa_katika_uchaguzi_wa_marudio_kenya_wapinzani_kuandamana_dhidi_ya_iebc
Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesaini mkataba na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kuhusu zabuni ya karatasi za kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 26, 2017 04:20 UTC
  • UN yajitosa katika uchaguzi wa marudio Kenya, wapinzani kuandamana dhidi ya IEBC

Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesaini mkataba na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kuhusu zabuni ya karatasi za kupigia kura kwa ajili ya uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26.

Katika barua ya IEBC kwa mrengo wa upinzani wa NASA ambao umekuwa ukisisitiza kuwa hautashiriki uchaguzi wa marudio iwapo masharti kadhaa uliyoyatoa hayatatekelezwa, Tume ya Uchaguzi imesema imefunga mkataba na UNDP, ambayo mbali na kubeba jukumu la kutafuta kampuni mpya ya kuchapisha karatasi za kupigia kura na fomu za matokeo ya uchaguzi, lakini pia imekubali kugharamia mchakato wote huo.

IEBC imesema ingawaje bado ina mkataba na kampuni ya al-Ghurair ya Dubai, lakini hatua hii ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa ni ahueni kwa mlipa kodi. Hata hivyo IEBC imesema kutokana na kubanwa na wakati, mkataba wake na kampuni ya teknolojia ya OT Morpho/Safran ya Ufaransa hautafutwa.

Rais Kenyatta (Kulia) na Odinga watakaochuana katika uchaguzi wa marudio Oktoba 26

Haya yanajiri huku viongozi wa mrengo wa upinzani wa Nasa wakitazamiwa hii leo kuongoza wafuasi wao katika maandamano ya kushinikiza kujiuzulu maafisa wa ngazi za juu wa IEBC, wanaotuhumiwa kuhusika katika uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi wa rais Agosti 8.

Hata hivyo Rais Uhuru Kenyatta hapo jana alisema hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kuishinikiza na kuifundisha IEBC namna ya kuendesha uchaguzi, huku akiwatahadharisha wataovuruga usalama na kuzusha ghasia katika maandamano ya leo.