Sep 29, 2017 03:23 UTC
  • OCHA: Hali ya mambo Jamhuri ya Afrika ya Kati inatia wasiwasi

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeeleza wasiwasi mkubwa ilionao kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika maeneo ya magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Najat Rochdi, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametangaza kuwa, hali ya kibinadamu katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo si ya kuridhisha.

Bi Najat Rochdi, amebainisha kuwa, kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba kwa mara nyingine tena hali ya kibinadamu katika maeneo hayo imezidi kuwa mbaya na kwamba, maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi baada ya makundi ya wabeba silaha kufanya mashambulio katika miji ya Niem na Bocaranga kwa lengo la kuidhibiti.

Najat Rochdi, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati

Afisa huyo wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametahadharisha kwamba, endapo kutazuka tena mapigano katika maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo basi hitajio la misaada ya kibinadamu katika hayo litaongezeka maradufu.

Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika dimbwi la mapigano na machafuko mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani rais wa nchi hiyo, François Bozizé. Katika mapigano hayo maelfu ya watu waliuawa wengi wao wakiwa ni Waislamu na wengine wengi kuwa wakimbizi. Hivi karibuni pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitahadharisha kuwa, yumkini Jamhuri ya Afrika ya Kati ikatumbukia tena katika mgogoro na machafuko makubwa ambayo yatavuruga jitihada za kurejesha amani na uthabiti katika nchi hiyo. 

 

Tags