Watu saba wauawa katika hujuma ya kigaidi karibu na Mogadishu, Somalia
Watu wasiopungua saba, wengi wakiwa wanawake wakulima, wameuawa karibu na mji mkuu wa Somalia kufuatia hujuma ya kigaidi huku mji huo ukiwa bado unaomboleza shambulizi la hivi karibuni lililoua mamia ya watu.
Taarifa zinasema hujuma ya leo Jumapili imejiri katika kijiji cha Daniga yapata kilomita 40 kaskazini magharibi mwa Mogadishu wakati bomu lilipolenga basi dogo la abiria.
Walioshuhudia wanasema walisikia mlipuko mkubwa ukitokea kisha miili ya waathirika ikawa imetapakaa mahala hapo ambapo basi lililolengwa liliharibiwa kabisa.
Eneo la Daniga liko karibu na maeneo yanayoshikiliwa na magaidi wa al Shabab, wanaofungamana na mtandao wa al-Qaeda na ambao wanalenga kuiangusha serikali halali ya nchi hiyo.
Oktoba 14 wiki iliyopita watu karibu 360 waliuawa katika hujuma za kigaidi zilizoulenga mji wa Mogadishu.
Ijapokuwa hadi sasa hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na shambulio hilo lakini viongozi wa serikali ya Somalia hawana shaka kuwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Al Shabab ndilo lililofanya shambulio hilo.