Wabunge wa upinzani Uganda warejesha 'hongo' ya kurefusha uongozi wa Museveni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35956-wabunge_wa_upinzani_uganda_warejesha_'hongo'_ya_kurefusha_uongozi_wa_museveni
Wabunge wanane wa upinzani wamerejesha kwenye hazina ya serikali fedha walizopokea kwa ajili ya kufanikisha muswada wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 26, 2017 08:07 UTC
  • Wabunge wa upinzani Uganda warejesha 'hongo' ya kurefusha uongozi wa Museveni

Wabunge wanane wa upinzani wamerejesha kwenye hazina ya serikali fedha walizopokea kwa ajili ya kufanikisha muswada wa kuondoa kikomo cha umri wa kugombea urais.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Kampala, Wabunge hao wamesema wanahisi 'sio sawa kimaadili' kupokea fedha hizo na kwamba hazikuweko kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Wabunge hao akiwemo Ibrahim Ssemujju, Muwanga Kivumbi, William Nzoghu, Angelina Osege, Robinah Ssentongo, Ana Adeke, Betty Aol na Moses Kasibante wamewataka wenzao wakiwemo wale wa chama tawala NRM kurejesha pesa hizo wanazozitaja kuwa 'chafu'.

Hivi karibuni, Chris Obore, Msemaji wa Bunge la Uganda alisema kila Mbunge wa nchi hiyo amepewa shilingi milioni 29 za nchi hiyo, sawa na dola elfu 8 za Marekani, ambazo watatumia katika shughuli za kupokea maoni ya wakazi wa maeneobunge yao kuhusu muswada huo.

Rais Museveni wa Uganda

Amesema kwa jumla serikali imetumia shilingi bilioni 13, sawa na dola milioni 3.3, kuwapa wabunge 445 wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kitendo ambacho kimewaghadhabisha sana wakosoaji wa serikali na wananchi walalahoi.

Muswada wa kuondoa kipengee cha umri wa kugombea urais kiliwasilishwa katika bunge la Uganda mwezi uliopita na hivi sasa wabunge wanajadiliana na wananchi wa kawaida kutaka kujua maoni yao. 

Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 73, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo mitatu, kisheria hafai kuwania tena urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 kwa sababu katiba ya Uganda imeainisha miaka 75 kuwa kikomo cha umri wa mtu anayetaka kugombea urais.