DRC: Tarehe ya uchaguzi inapangwa na tume, sio Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36000-drc_tarehe_ya_uchaguzi_inapangwa_na_tume_sio_marekani
Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo CENI yenye mamlaka na uwezo wa kupanga tarehe ya uchaguzi nchini na wala sio Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 28, 2017 04:33 UTC
  • DRC: Tarehe ya uchaguzi inapangwa na tume, sio Marekani

Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini humo CENI yenye mamlaka na uwezo wa kupanga tarehe ya uchaguzi nchini na wala sio Marekani.

Kauli hiyo imetolewa baada ya Nikki Haley, balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ambaye yuko katika safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika kusema kuwa, sharti Kongo DR iandae uchaguzi mkuu mwaka ujao 2018, vinginevyo Marekani haitaunga mkono wala kufadhili mchakato wa uchaguzi huo ukifanyika baada ya mwaka ujao.

Lambert Mende, Msemaji wa serikali ya DRC amesema: "Sio kazi ya serikali, wala Bi. Haley kupanga mambo ya uchaguzi nchini, kwa hiyo sidhani kama tunaweza kukubali kuwekwa chini ya mashinikizo na masharti ya aina hii."

Haley ambaye jana Ijumaa alikutana na maafisa wa CENI, wakuu wa vyama vya siasa na viongozi wa Kanisa Katoliki alisema Marekani haitakubali uchaguzi ufanyike baada ya mwaka ujao 2018. Aidha alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Joseph Kabila kwa takriban dakika 90 hivi.

Nikki Haley, balozi na mwakilishi wa Marekani katika UN

Hata hivyo mwanadiplomasia huyo wa Marekani hakufafanua zaidi hatua itakayochukuliwa na Washington iwapo uchaguzi huo utakosa kufanyika.

Mapema mwezi huu, CENI ilitangaza kuwa, hakuna uchaguzi utakaofanyika nchini humo hadi katikati ya mwaka 2019, hatua ambayo ilikabiliwa na malalamiko makubwa ya wapinzani wanaosema ni njama za Rais Kabila wa nchi hiyo za kuendelea kubakia madarakani.