Mbunge wa CCM Lazaro Nyalandu ajiuzulu; atangaza kuhamia Chadema+Sauti
Mbunge wa chama tawala nchini Tanzania CCM Lazaro Nyalandu amejiuzulu wadhifa wake, na kusema kwamba anataka kuhamia chama cha upinzani Chadema.
Bw Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) na aliyewahi kuwa Waziri wa Mali Asili na Utalii katika serikali ya awamu ya nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kupitia taarifa kwamba amejuzulu nyadhifa zake zote ndani ya chama cha mapinduzi CCM ikiwemo Ubunge.
Nyalandu ambaye kabla ya maamuzi hayo ya kujiuzulu alikuwa Mbunge wa Singida Kaskazini amesema amechukua uamuzi huo kutokana na kutokuridhishwa na mwendo wa siasa nchini Tanzania, ukiukwaji wa haki za kibinaadamu, ongezeko la vitendo vya kidhalimu dhidi ya raia na kutokuwepo kwa mipaka baina ya mihimili ya dola - Serikali, Bunge na Mahakama.
Katika taarifa yake ya kujiuzulu aliyoiweka katika ukurasa wake wa Facebook, Nyalandu amesisitiza umuhimu wa nchi hiyo kupata katiba mpya.
"Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali," amesema.