Kanali aliyeasi jeshi la DRC ajisalimisha baada ya mapigano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36183-kanali_aliyeasi_jeshi_la_drc_ajisalimisha_baada_ya_mapigano
Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumapili wamepigana na wafuasi wa kanali aliyeasi jeshi katika mji wa Bukavu mashariki mwa nchi hiyo na baada ya hapo kanali huyo akajisalimisha kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 05, 2017 11:20 UTC
  • Kanali aliyeasi jeshi la DRC ajisalimisha baada ya mapigano

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jumapili wamepigana na wafuasi wa kanali aliyeasi jeshi katika mji wa Bukavu mashariki mwa nchi hiyo na baada ya hapo kanali huyo akajisalimisha kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa Jeshi la DRC katika eneo la Kivu Kusini Dieudonne Kasereka amesema mapigano yalianza pale polisi walipotaka kumpokonya silaha Kanali Abbas Kayonga, ambaye alifutwa kazi Alhamisi.

Kufuatia mapigano makali, Kayonga, ambaye zamani alikuwa katika kundi la waasi lililopokonywa silaha na kuingizwa katika jeshi, alijisalimisha katika kituo cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Kasereka amesema Kayonga amejisalimisha na wafuasi wake 17 huku akiongozea kuwa watu kadhaa wameuawa katika mapigano hayo ingawa idadi kamili haijulikani.

Rais Joseph Kabila

Usalama umekuwa ukizirota kote DRC tokea Disemba mwaka jana wakati Rais Joseph Kabila alipokataa kuachia ngazi pamoja na kuwa muhula wake ulikuwa umemalizika kikatiba.

Eneo la Mashariki mwa DRC kwa miongo kadhaa limekuwa kitovu cha mapigano kutokana na utajiri wake wa madini.