Watu 18 wakabiliwa na tuhuma za kufanya ukatili wa kingono Congo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36391-watu_18_wakabiliwa_na_tuhuma_za_kufanya_ukatili_wa_kingono_congo_dr
Watu 18 akiwemo afisa mmoja wa serikali ya kikanda wanakabiliwa na tuhuma za kufanya ukatili wa kingono huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
(last modified 2026-04-26T10:08:53+00:00 )
Nov 14, 2017 12:22 UTC
  • Watu 18 wakabiliwa na tuhuma za kufanya ukatili wa kingono Congo DR

Watu 18 akiwemo afisa mmoja wa serikali ya kikanda wanakabiliwa na tuhuma za kufanya ukatili wa kingono huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti zinasema kuwa juhudi zilizoanzishwa na jumuiya za kiraia na uchunguzi wa mafaili ya ukatili wa kingono katika mahakama ya Kavumu huko katika mkoa wa Kivu Kusini vimehuisha matumaini ya kutekelezwa sheria dhidi ya wahalifu wa ukatili wa kingono mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Watu hao 18 akiwemo Fredric Batumbeki, afisa wa serikali ya kikanda katika eneo la Kavumu wanakabiliwa na mashtaka ya kunajisi wasichana 40 katika kipindi cha kati ya mwaka 2013 na 2016. Watu hao pia wanakabiliwa na mashtaka ya kushirikiana na kundi moja la waasi dhidi ya serikali ya Congo. 

Ukatili wa kingono umekithiri Congo DR

Watuhumiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka ya kunajisi watoto kadhaa waliokuwa na umri wa kati ya miaka 8 na 12 na kwamba watoto wawili miongoni mwa wahanga hao wamefariki dunia kutokana na ukatili huo. 

Wataalamu wanasema ubakaji na kunajisi wanawake vinatumiwa kama silaha ya vita katika mapigano ya ndani huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Kutokana na hali hiyo mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa ameitaja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuwa ni "mji mkuu wa ukatili wa kingono duniani".