Besigye akamatwa tena, polisi Uganda yatumia vitoa machozi kuzima mkutano wa upinzani
Kwa mara nyingine tena polisi ya Uganda imemtia mbaroni kinara wa upinzani nchini humo Kizza Besigye, kwa tuhuma za kuitisha mkutano wa hadhara pasina kibali cha vyombo vya usalama.
Habari zinasema kuwa, Besigye alikamatwa jana muda mfupi kabla ya kuhutubia mkusanyiko wa wafuasi wa chama cha upinzani cha FDC katika wilaya ya Mbarara, magharibi mwa mji mkuu Kampala.
Besigye, dereva wake pamoja na Ingrid Turinawe, Katibu wa Uenezi wa chama cha FDC walikamatwa walipokuwa wakielekea katika uwanja wa Kakyeka ambako wafuasi wao walikuwa wamekusanyika, na kwa sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mbarara.
Maafisa wa polisi wa Uganda walitumia mabomu ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuutawanya mkusanyiko huo wa wapinzani.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Besigye, maafisa wawili wa ngazi za juu wa chama cha FDC pamoja na Kato Lubwama, Mbunge wa Rubaga Kusini na mwenzake wa Butambala, Muwanga Kivumbi walikamatwa mjini Kampala kwa kuongoza maandamano ya kupinga juhudi za kuondoa kipengee cha katiba kilichoweka kikomo cha umri wa kugombea urais.
Wapinzani wanaitizama hatua hiyo kama mpango wa kumfungulia njia Rais Yoweri Museveni endelee kubakia madarakani.