Kipindupindu chauwa watu 50 Kongo katika muda wa wiki moja
Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ugonjwa wa Kipindupindu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ametangaza kuwa watu 50 wamefariki dunia nchini humo baada ya kuambukizwa ugonjwa huo katika muda wa wiki moja.
Didier Bompange amesema katika mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa na Wizara ya Afya ya Kongo kuwa watu 1990 waliripotiwa kuambukizwa ugonjwa wa kipindupindu nchini humo kuanzia tarehe 6 hadi 12 mwezi huu na kwamba 50 miongoni mwao wameaga dunia katika kipindi cha wiki moja tu.
Bompange amesema kuwa, watu zaidi ya 45,000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameambukizwa kipindupindu kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu na wengine 918 wameaga dunia.
Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ugonjwa wa Kipindupindu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameashiria mlipuko wa ugonjwa huo katika mikoa 22 kati ya 26 ya nchi hiyo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za dharura za kukabiliana na maradhi hayo. Afisa huyo wa afya wa Kongo ameongeza kuwa mkoa wa Kasai katikati mwa nchi umeathirika zaidi na maambukizo ya kipindupindu.