Waasi wa Mai-Mai washambulia ngome za jeshi mashariki mwa DRC
Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mkoa wa Kivu Kusini ulioko mashariki mwa nchi hiyo amesema kuwa, waasi wa Mai-Mai wameshambulia ngome za jeshi katika mji wa Kilembwe.
Louis-Claude Tshimwanga, msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mkoa wa Kivu Kusini amewaambia waandishi wa habari kwamba, waasi wa Mai-Mai wamemuua mwanajeshi mmoja katika mashambulio yao hayo.
Ameongeza kuwa, jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limerudi nyuma kutoka katika mji huo ili kuzuia kutokea maafa zaidi na kwamba, kwa sasa mji huo unadhibitiwa na waasi hao wa Mai-Mai.
Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameeleza kuwa, mashambulio ya waasi hao yamezusha wasiwasi na wahaka mkubwa miongoni mwa raia na kwamba, baadhi ya wakazi wa mji huo wameyakimbia makazi yao.
Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likishuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Ukosefu wa usalama katika maeneo hayo umewalazimisha raia wengi kuyakimbia makazi yao na hivyo kuwa wakimbizi.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kushindwa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuyatokomeza makundi ya wanamgambo ndiko kulikoshadidisha ukosefu wa amani na uthabiti mashariki mwa nchi hiyo.