Maelfu ya familia zakimbia mashariki mwa Congo DR kwa kuhofia usalama wao
Maelfu ya wakazi wa mkoa wa Kivu Kaskazini huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamekimbia makazi yao kwa kuhofia mashambulizi yanayofanywa na makundi ya wanamgambo katika eneo hilo.
Jumuiya isiyo ya serikali ya ARDA imetangaza kuwa, familia elfu tatu za maeneo ya Masisi na Walikale zimelazimika kukimbia makazi yao katika mwezi huu wa Novemba kutokana na mashambulizi ya makundi ya wanamgambo.
Ripoti ya taasisi hiyo imesisitiza kuwa makundi kadhaa ya wapiganaji wenye silaha yaliyoanzishwa katika maeneo hayo mwezi Machi mwaka huu yamekuwa yakipigana mara kwa mara na kusababisha ghasia na machafuko.
Jumuiya ya ARDA imesema kuwa, makundi hayo yamekuwa yakipora mali za hospitali na vituo vya afya katika mkoa wa Kivu Kaskazini na kuharibu makazi ya raia.
Mashambulizi hayo yamewazuia wanafunzi kwenda mashuleni na wakulima wamelazimika kubakia majumbani na kuacha shughuli zao kwa kuhofia usalama na maisha yao.
Maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekuwa yakisumbuliwa na machafuko na mapigano ya mara kwa mara tangu miaka 20 iliyopita.