Nov 27, 2017 15:15 UTC
  • Kamanda wa kundi moja la waasi atiwa mbaroni Darfur Sudan

Wizara ya Ulinzi ya Sudan imetangaza habari ya kutiwa mbaroni kamanda wa kundi moja la waasi wa eneo la Darfur la magharibi mwa Sudan kwa tuhuma za kuvunja haki za binadamu.

Wizara hiyo imetangaza leo kuwa, kikosi kimoja cha jeshi la Sudan kimemtia nguvui Musa Helal, kamanda wa kundi la waasi wa Darfur katika mkoa wa Darfur Kaskazini kwa tuhuma za kuvunja haki za binadamu.

Kabla ya hapo Umoja wa Mataifa ulikuwa umemtuhumu Musa Helal kuwa anaongoza kundi linalovunja haki za binadamu katika jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan.

Wanajeshi wa Sudan

 

Tangu mwaka 2003 jimbo la Darfur limekumbwa na machafuko na mapigano ya silaha huku makabila ya eneo hilo yakilalamika kuwa serikali imewabagua. Mapigano makali ya umwagaji wa damu yamekuwa yakiripotiwa kwenye jimbo hilo kwa miaka mingi sasa.

Machafuko hayo yameshapelekea watu 300 kuuawa na karibu milioni mbili na nusu kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.

Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa zinaendesha operesheni ya kulinda amani katika jimbo hilo chini ya mwavuli wa kikosi cha UNAMID.

Kwa kiasi fulani UNAMID imefanikiwa kurejesha hali ya utulivu kwenye jimbo hilo ingawa hadi hivi sasa kumekuwa kukiripotiwa mapigano ya hapa na pale baina ya pande hasimu.

Tags