Wakimbizi wa Burundi nchini Tanzania wanakabiliwa na hali mbaya: UNHCR
Maelfu ya wakimbizi wa Burundi wanaishi katikia hali mbaya kwenye kambi za wakimbizi nchini Tanzania kwa sababu ya uhaba wa fedha. hayo yamesemwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.
Kwa mujibu wa shirika hilo, upungufu wa fedha za kufadhili miradi ya kuwasaidia wakimbizi hao imesababisha wengi kuendelea kuishi katika mahema ya dharura baadhi yao tangu miaka miwili iliyopita walipowasili kwenye kambi hizo za Nyarugusu na Nduta mkoni Kigoma, magharibi mwa Tanzania.
UNHCR inasema, madhila yamezidishwa na kuingia kwa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kufuatia machafuko ya karibuni. Hivi sasa UNHCR na washirika wake wameanza kuwahamishia wakimbizi hao kwenye makazi ya mpito na kusaidia mradi utakaowawezesha kujenga makazi yao. Makazi hayo ya mpito ni bora zaidi lakini yanapatikana tu kwa wakimbizi waliowasili hivi karibuni. Patrick Mutai, afisa wa makazi wa UNHCR kwenye kambi hizo amesema, wakimbizi wanapohamia kwenye makazi hayo wanatumia matofali ya matope na kuanza ujenzi ili kuboresha makazi yao ya kudumu au ya muda.
Ingawa makazi hayo yanatoa matumaini, UNHCR inasema fedha zaidi za ufadhili zinahitajika ili kuwasaidia maelfu ya wakimbizi ambao bado wanaishi kwenye hali mbaya.
Kuna wakimbizi takribani 250,000 wa Burundi katika kambi mbali mbali za wakimbizi nchini Tanzania. Burundi ilitumbukia katika machafuko mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka 2015 baada ya chama tawala cha CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza, kugombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita kwa mara ya tatu mfululizo, machafuko ambayo yalishika kasi zaidi mjini Bujumbura.
Wapinzani waliitaja hatua ya Rais Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi huo kwamba, ilikiuka katiba na hati ya makubaliano ya amani ya Arusha Tanzania. Hata hivyo serikali ya Burundi inasisitiza kuwa haijakiuka mapatano ya Arusha.