Mlipuko wa 'bacteria' waua makumi ya watu nchini Afrika Kusini
Kwa akali watu 36 wamepoteza maisha kutoka na mlipuko wa vijidudumaradhi (bacteria) vinavyoathiri chakula nchini Afrika Kusini.
Waziri wa Afya nchini humo, Aaron Motsoaledi amesema mbali na vifo hivyo, kesi 557 za walioathirika na bacteria hiyo aina ya Listeria monocytogenes zimeripotiwa.
Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari mjini Pretoria kuwa, vijidudumaradhi hivyo vinaenezwa kupitia maji, mchanga na mimea, huku akitoa indhari kwa wanachi dhidi ya kula chakula kilichoathiriwa na bacteria hiyo, hususan nyama, matunda na aina mbalimbali za mboga za majani.
Amefafanua kuwa, bacteria hiyo aina ya Listeria monocytogenes inaweza kumfanya muathiriwa ajihisi kama ana mafua, kuvurugika mtiririko wa damu na pia kumsabababishia matatizo ya ubongo.
Shirika la Afya Duniani WHO limewataka wananchi wa Afrika Kusini kutumia maji safi ya kunywa, kunawa mikono mara kwa mara na kutenganisha chakula kibichi na kilichopikwa.