Jean-Pierre Lacroix: Mapigano ya kikabila Sudan Kusini yamechochea hali ngumu
Mkuu wa operesheni za kusimamia amani za Umoja wa Mataifa amesema kuwa, mapigano ya kikabila katika nchi ya Sudan Kusini yamekuwa na nafasi kubwa katika kuifanya hali ya mambo ya nchi hiyo izidi kuwa mbaya.
Jean-Pierre Lacroix amesema hayo alipokuwa akiwasilisha ripoti ya siku 90 ya Katibu Mkuu wa umoja huo kuhusu hali ya usalama na kibinadamu nchini Sudan Kusini.
Mkuu wa opresheni za kusimamia amani za Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hadi sasa watu wengi wamepoteza makazi yao tangu mapigano yaanze nchini humo mwaka 2013 huku ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo uporaji, uchomaji wa nyumba na ukatili wa kingono vikishamiri katika maeneo yote ya nchi hiyo.
Jean-Pierre Lacroix ametaja mambo kadhaa ambayo amesema yanapaswa kuzingatiwa ili kuboresha hali ya amani na usalama huko Sudan Kusini. Amesema kuwa, kuzingatia haraka usitishaji mapigano kwa pande zote kwenye mzozo, kushughulikia changamoto za watoa misaada katika kusambaza huduma hizo na kuondoa vikwazo dhidi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS ni baadhi ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele katika juhudi za kurejesha amani huko Sudan Kusini.
Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko na mapigano kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani, Riek Machar tangu mwaka 2013. Vita vya ndani nchini humo vimepelekea kuuawa maelfu ya raia na wengine zaidi ya milioni nne kulazimika kuwa wakimbizi. Mapigano yanaendelea nchini Sudan Kusini katika hali ambayo, mgogoro wa kisiasa na vita vimepelekea kutokea mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika nchi hiyo.