UN: Askari 14 wa kulinda amani Congo DR wameuawa
Askari 14 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa wameuawa na wengine 40 kujeruhiwa katika shambulizi lililofanyika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Hayo yamethibitishwa na mkuu wa operesheni za kusimamia amani za Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix ambaye amesema shambulizi hilo limefanyika katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Lacroix ameongeza kuwa, amekasirishwa sana na shambulizi hilo na kwamba operesheni ya kuwashughulikia askari wa Umoja wa mMataifa waliopatwa na masaibu katika shambulizi hilo ilikuwa ikiendelea.
Hata hivyo afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa hakuweka wazi ni nani au kundi lipi lililofanya mashambulizi hayo dhidi ya askari wa kimataifa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Itakumbukwa kwamba, kikosi cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndicho kikubwa zaidi duniani na lengo lake ni kupunguza idadi ya makundi ya waasi na yanayobeba silaha katika nchi hiyo kubwa na yenye utajiri wa madini ya katikati mwa Afrika.