Mgogoro mkubwa wa Congo DR ndio uliopuuzwa zaidi mwaka 2017
(last modified Wed, 20 Dec 2017 03:43:47 GMT )
Dec 20, 2017 03:43 UTC
  • Mgogoro mkubwa wa Congo DR ndio uliopuuzwa zaidi mwaka 2017

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na mashirika ya misaada ya kibinadamu umebaini kuwa, mgogoro mkubwa wa kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio uliopuuzwa zaidi katika mwaka huu unaomalizika wa 2017.

Uchunguzi wa mashirika hayo umesema kuwa, mgogoro wa kibinadamu wa Congo ambao umefunikwa na vita vya Syria na maafa ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar haukuakisiwa sana katika vyombo vya habari mwaka huu licha ya ukatili na unyanyasaji wa kutisha ulioshuhudiwa katikati mwa nchi hiyo.

Jamhuri ya Afrika ya Kati na maafa ya watu wa Yemen waliozongwa na masaibu ya mashambulizi ya Saudi Arabia na washirika wake vinashika nafasi ya pili na tatu katika orodha ya migogoro mikubwa ya kibinadamu iliyopuuzwa zaidi katika mwaka huu.

Saudi Arabia inaendelea kuua watoto wa Yemen bila ya huruma

Mark Smith ambaye ni afisa wa shirika la misaada ya kibinadamu la World Vision anasema mgogoro wa kibinadamu wa Congo DR umekuwa ukiendelea bila ya kufichuliwa na kuwekwa wazi na yeyote na kwamba, ukubwa wa ukatili unaofanywa dhidi ya watoto katika maeneo ambayo ni vigumu kuyatembelea ni mambo ambayo hayatasawariki.

Mashirika ya misaada ya kibinadamu yameongeza kuwa uasi dhidi ya serikali ya Kinshasa katika eneo la Kasai umewalazimisha watu zaidi ya milioni moja kuwa wakimbizi na kwamba njaa na uhaba wa chakula unahatarisha maisha ya mamia ya maelfu ya watoto nchini humo. 

Raia wa Congo DR wanaendelea kuuawa ovyo

Mashirika hayo pia yamepokea ripoti za mauaji ya umati, ubakaji na kukata vichwa vya watu. Pia kuna ripoti za mashambulizi ya kutisha dhidi ya watoto wachanga na watoto wadogo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Vilevile nchi hiyo inashuhudia maafa ya kusajiliwa watoto wadogo kama wapiganaji katika makundi yenye silaha.

Tags