UN yaimarisha usalama kambi walikouawa walinda amani wa Tanzania huko DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i37933-un_yaimarisha_usalama_kambi_walikouawa_walinda_amani_wa_tanzania_huko_drc
Umoja wa Mataifa umesema kambi ya Semuliki ya Kivu Kaskazini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambayo ilishambuliwa na waasi tarehe 7 mwezi huu na kusababisha vifo vya walinda amani 14 wa Tanzania na wengine 44 kujeruhiwa sasa inaimarishwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 22, 2017 03:49 UTC
  • UN yaimarisha usalama kambi walikouawa walinda amani wa Tanzania huko DRC

Umoja wa Mataifa umesema kambi ya Semuliki ya Kivu Kaskazini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambayo ilishambuliwa na waasi tarehe 7 mwezi huu na kusababisha vifo vya walinda amani 14 wa Tanzania na wengine 44 kujeruhiwa sasa inaimarishwa.

Mkuu wa operesheni za ulinzi wa amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix amesema hayo baada ya kuzuru eneo hilo na kukagua uimarishwaji ulinzi wakati huu uchunguzi wa tukio hilo ukisubiriwa kwa hamu.

Akihojiwa na Radio Okapi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko DRC, MONUSCO, Lacroix amezungumzia pia uchunguzi wa tukio hilo na kusema utafanyika kwa mbinu ambazo zinatakiwa. Hitimisho na mapendekezo  yake yatachambuliwa kwa kina na kuzingatiwa kwa hali ya juu na kwa haraka iwezekanavyo.

Askari 14 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  waliuawa mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba, na 44 wengine walijeruhiwa katika kambi hiyo kufuatia hujuma ya waasi wa ADF.

Askari wakiwa wamebeba jeneza la mwenzao aliyeuawa DRC

Tukio hilo lilitokea Desemba 7, 2017 katika kambi ndogo iliyoko katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu.

Askari waliouawa walikuwa ni sehemu ya askari 3,000 wa timu ya kulinda amani ya umoja wa mataifa MONUSCO yenye askari kutoka Tanzania, Malawi na Afrika Kusini.