Maandamano ya kulalamikia mfumko wa bei yashtadi Tunisia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38733-maandamano_ya_kulalamikia_mfumko_wa_bei_yashtadi_tunisia
Mtu mmoja ameuawa, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya wananchi wa Tunisia wanaolalamikia mfumko wa bei za bidhaa na kile wanachokitaja kama 'bajeti isiyo ya uadilifu'.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2018 12:21 UTC
  • Maandamano ya kulalamikia mfumko wa bei yashtadi Tunisia

Mtu mmoja ameuawa, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya wananchi wa Tunisia wanaolalamikia mfumko wa bei za bidhaa na kile wanachokitaja kama 'bajeti isiyo ya uadilifu'.

Maandamano hayo yalianza jana katika mji mkuu Tunis, na sasa yameenea katika maeneo mengine ya nchi.

Hamma Hammami, kiongozi wa muungano wa upinzani wa Popular Front amenukuliwa na vyombo vya habari akisema viongozi wa vyama vya upinzani wamefanya mkutano hii leo na wameafikiana kuendeleza maandamano hayo hadi serikali ifute bajeti hiyo ya mwaka wa fedha 2018/2019.

Kwa mujibu wa wanaharakati wa haki za binadamu nchini Tunisia, polisi wametumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaopinga kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali.

Watunisia walalamikia ugumu wa maisha

Mamia ya watu wametiwa mbaroni katika maandamano hayo. Mkuu wa Usalama wa Taifa, Walid Ben Hakima amekanusha madai kuwa polisi ndio waliomuua mtu aliyekuwa na umri wa miaka 43 katika eneo la Tebourba, magharibi mwa Tunis na kusisitiza kuwa mtu huyo alikuwa na matatizo ya pumu.

Amesema maafisa usalama 11 wamejeruhiwa kwa kurushiwa mawe wakikabiliana na waandamanaji waliozusha vurumai na kuharibu mali za umma.

Kadhalika mamia ya watu wamefanya maandamano katika mji wa Sidi Bouzid, sehemu ilipoanzia harakati ya mwamko iliyopelekea kung'olewa madarakani, dikteta Zainul Abiddine Ben Ali mwaka 2011.