Chama cha ACT Wazalendo Tanzania chataka Trump achukuliwe hatua kali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38943-chama_cha_act_wazalendo_tanzania_chataka_trump_achukuliwe_hatua_kali
Chama cha ACT Wazalendo cha nchini Tanzania kimetaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani kufuatia hatua yake ya kutoa matamshi ya chuki dhidi ya mataifa ya Afrika na raia wanaotoka bara la Afrika.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jan 14, 2018 01:21 UTC

Chama cha ACT Wazalendo cha nchini Tanzania kimetaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Rais Donald Trump wa Marekani kufuatia hatua yake ya kutoa matamshi ya chuki dhidi ya mataifa ya Afrika na raia wanaotoka bara la Afrika.

Takwa hilo limetolewa na Mkurugenzi wa Kamati ya Masuala ya Kigeni katika chama hicho Vennace Msebo katika taarifa yake.

''Kwa niaba ya chama, ninalaani pakubwa matamshi ya ubaguzi wa rangi ya rais Donad Trump. Kuwaita Waafrika na watu kutoka Afrika wachafu na wanaotoka katika "Shimo la Kinyesi" ni ubaguzi wa rangi na tabia ya chuki ya utawala mpya wa Marekani kwa bara Afrika na ulimwengu hautanyamaza'', alisema.

Ameongeza kuwa, chama hicho kinapongeza hatua ya taifa la Botswana kuhusu suala hilo na kinajivunia kwamba taifa la Botswana limekuwa mstari wa mbele katika kushutumu kwa vitendo suala lolote linalokandamiza Afrika na watu wake.

Aidha amesema: "Vilevile tunapongeza taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na hatua iliyochukuliwa na mabalozi wa Afrika mjini Washington na tunaunga mkono hatua hiyo.

Afisa huyo wa ACT-Wazalendo pia ameyataka mataifa ya bara Afrika kutathmini matamshi hayo ya rais wa Marekani kama muamko kwa mataifa ya Afrika ili kujiimarisha kiuchumi na kukabiliana na umasikini kwa lengo la kujisimamia.