Ethiopia yafuta mashtaka dhidi yawafungwa wa kisiasa
Mwanasheria Mkuu wa Ethiopia amesema kuwa serikali ya nchi hiyo imefuta mashtaka dhidi ya mmoja wa viongozi wa kambi ya upinzani na wapinzani wengine 528 wanaoshikiliwa katika magereza ya nchi hiyo.
Wapinzani hao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kuchochea machafuko yaliyoikumba nchi hiyo kati ya mwaka 2015 na 2016.
Watu zaidi ya 700 waliuawa katika machafuko yaliyotokea katika eneo la Oromo wakati watu wa kabila la Oromia walipokuwa wakiandamana kupinga sera za serikali ya Addis Ababa.
Waandamanaji hao waliilaumu serikali ya Ethiopia kuwa iwasaidia mabepari na mabwanyenye kupora ardhi zao na kukandamiza wanaharakati wa kisiasa.
Idadi kamili ya wafungwa wa kisaisa wanaoshikiliwa katika jela za Ethiopia haijulikani lakini aghlabu yao walikamatwa katika ghasia na maandamano dhidi ya serikali ya nchi hiyo katika maeneo ya Amhara na Oromo tangu mwezi Agosti mwaka 2015 wakilalamikia kubaguliwa.

Watetezi wa haki za binadamu wanasema kuwa karibu wafungwa elfu mbili wa kisiasa wangali wanashikiliwa katika jela za Ethiopia.
Siku chache zilizopita Waziri Mkuu wa Ethiopia alitangaza mpango wa serikali wa kufuta mashitaka dhidi ya wafungwa wote wa kisiasa sambamba na kufunga jela ya kuogofya ambako wafungwa hao walikuwa wanazuiliwa.