Polisi Sudan watumia mabomu na bakora kuzima maandamano
Maafisa usalama nchini Sudan wametumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, wanaolalamikia ughali wa maisha na hali ngumu ya kiuchumi.
Mamia ya waandamanaji wamekusanyika leo Jumanne nje ya Ikulu ya Rais katika mji mkuu Khartoum, kuitikia mwito wa kiongozi wa upinzani wa Chama cha Kikomunisti cha Sudan, aliyewataka waendelee na maandamano hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa.
Polisi wametumia mabomu ya kutoa machozi kuzima maandamano hayo, huku baadhi yao wakiwakabili na kuwapiga bakora waandamanaji.
Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za, 'Hapana kwa njaa! na Hapana kwa mfumko wa bei! Maandamano hayo yameenea Sudan nzima kulalamikia hatua ya serikali ya kupandisha bei ya bidhaa muhimu.
Hadi hivi sasa mwanafunzi mmoja wa shule ya sekondari ameshauawa na watu wengine sita kujeruhiwa katika maandamano hayo yaliyoanza Jumatatu iliyopita.
Duru za habari zimedokeza kuwa, Rais Omar al Bashir wa Sudan anafikiria kuivunja serikali ya Waziri Mkuu Bakri Hassan Saleh kutokana na kushindwa kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi na kupanda bei ya bidhaa muhimu kama mkate na umeme na hali mbaya ya kushuka thamani ya sarafu ya nchi hiyo.